Home Search Countries Albums

Tatoo Ya Asili

DIZASTA VINA

Tatoo Ya Asili Lyrics


Amezongwa na zimwi
Alisikia jirani akitoa hoja kwa kijiji
Sababu ya kukosa elimu ya maambukizi
Walihisi kurogwa ndio sababu ya gonjwa la Ukimwi
Huyo ni mgonjwa jamani
Kama wagonjwa wengine alisema mwalimu
Mwenyekiti alimwambia kaa kimya
Sio unaropoka kama mwendawazimu
Elimu ya mwalimu ilikuwa nuru potevu
Nuru ambayo haifiki gizani
Ikawekwa idhini mezani kuuwa mizimu imechukia
Mgonjwa afukuzwe kijiji cha mbali
Akasindikizwa njiapanda
Mwisho wa kijiji mwanzo wa msitu mkubwa wa Sanza
Alitengwa kama walivyotengwa wengi
Kwa mila na desturi zilizoanza tangu enzi
Kibuyu cha maji furushi la matunda
Na makubazi yaliyoalika funza
Hakuna hodi inapofika kiama
Mama na nyika nyika na mama
Na alikuwa peke yake na ule mzigo mdogo mgongoni
Wasiwasi usoni mtoto tumboni
Alitamani matawi yaanguke yamtunze
Dhidi ya baridi ya mji uliosahaulika na Wabunge
Umauti aliuhisi
Alijitazama na hakuona tofauti na maiti
Alilia peke yake porini huku sauti yake
Ikisindikizwa na sauti za fisi
Wadudu wenye sumu nyingi walimvizia
Alikutana na visiki alipotaka njia
Mvua kubwa ilinyesha kuonyesha
Hata hali ya hewa ilimsaliti pia
Alivuka salama mpaka ng'ambo
Akajikongoja mpaka kando
Kando kwenye mti mkubwa uchungu ulimshika
Alizaliwa mtoto mdogo huku mama anakufa
Ujinga uliotamalaki kwa kijiji
Ndio ujinga uliomnyima haki ya kuishi
Alipambana mpaka ilifika tamati Pumzi
Akamwacha mwanae na zawadi ya virusi
Natoa nukuu kariri
Mtoto alifunikwa na nguo kuu kuu kwenye mwili
Alikuwa na madoa makuu mawili
Katikati ya mgongo mfano wa tatuu ya asili

Ninatokwa na mate
Alisikika kijana akitoa hoja kwa wenzake
Waliopanga foleni kwenye chumba chenye mwanga
Hafifu kila mmoja akiingoja zamu yake
Walikuwa vijana sita wenye umri wa shule
Usipojua thamani utahisi wanaivuta pumzi ya bure
Alilala msichana kati ya hawa
Kwenye matandiko machafu yalioarika chawa
Jamani huyu ni mtoto bado
Alisikika mmoja aliyeegemea ndoo ndogo kando
Walimfokea alipokataa kushiriki tukio
Wakimfananisha na Mbwa asiyevuka uzio
Walimvua msichana nguo zake za mwili
Walimpiga alipojaribu kuficha sehemu zake za siri
Alibakwa kama walivyobakwa wengi
Kwa tabia za vijana zilizoanza tangu enzi
Hawakujua kuhusu mpaka wa hamu
Halali na haramu kila mmoja alimbaka kwa zamu
Alitendewa uasi
Kwa vijana walioshindwa kulelewa na wazazi
Mfano wa mlo wa hija walimfakamia
Aliliona giza alipotaka njia
Alisema imetosha ila hakuna aliyemsikia
Maana wengine dada zao walibakwa pia
Alitakiwa awe nyumbani labda
Kalala kakumbatia Mwanasesere kitandani labda
Alilia na sauti yake haikukidhi
Kwa sababu hata mji ulisahaulika na polisi
Msimuliaji toka chini nalia juu
Nasimulia yaliyotukia huruma inaniingia
Lakini sina cha kufanya kwa sababu
Kazi yangu mi' kusimulia tu
Kuta zingeongea zingeusema huu ukatili
Wa maumivu ya juu ya mwili
Kuta zingesema alikuwa na madoa makuu mawili
Kati' ya mgongo mfano wa tatuu ya asili

Enjoy Synced Lyrics With Our Mobile App

Download on Google PlayGet it on App Store

WATCH VIDEO

ABOUT THIS SONG


Release Year : 2023


Album : Tatoo Ya Asili (Single)


Added By : Farida

SEE ALSO

AUTHOR

DIZASTA VINA

Tanzania

Dizasta Vina  (real name Edger Vicent) aka "The Black Maradona" is  Hip-hop arti ...

YOU MAY ALSO LIKE